Friday, June 1, 2012

#ZANZIBAR REVEALED

 kuna dhana ya kuwa karume aliuawa kulinda muungano, mazingira yote ya kuuawa kwa karume haiihusishi tanganyika kwa namna moja ama nyengine katika mauaji hayo na kwamba ni wananchi walichoshwa na serikali yao. kinachotokea leo zanzibar, ni msingi mbovu wa utawala wa tokea awali na kamwe tanganyika isihusishwe. 

jarida moja la kila mwezi 'Africa Events' la Agosti 1992 (uk. 27) ,linadai sababu za kuuawa kwa Karume zilikuwa za kibinafsi kwa njia ya kulipa kisasi. Inaelezwa kwamba Muhammed Hamud, mtoto wa Hamud Muhammed Hamud, aliyetiwa kizuizini miezi michache baa­da ya mapinduzi ya 1964 akituhumiwa kutaka kuipindua Serikali ya Karume.
Miaka, rnichache baadaye, Luteni Hamud Muhammed Hamud akiwa katika mafunzo ya kijeshi huko Tashkent (Urusi ya zamani), aliambiwa na mwanafun­zi mwenzake kwamba mzee Hamud alinyongwa na Karume akiwa kizuizini hila kufunguliwa mashtaka. Kwa taarifa hiyo, Luteni Hamud alisikika akiapa ange­muua Karume akirejea Zanzibar.
Taarifa ya kusudio la Hamud la kuua ilifikishwa kwa vyombo vya usalama Visiwani na wenzake, lakini hakukamatwa wala kuwekwa wa chini ya uchunguzi mkali ali­porejea Zanzibar; badala yake ali­pandishwa cheo kuwa luteni na Karume mwenyewe.
Jarida hili halisemi lolote juu ya raja Ali Khatibu Chwaya na ko­plo mwingine juu ya kushiriki kwao katika mauaji haya. Hata hivyo,. Kushiriki kwao kunaelekea kutetea dhana ya pili kwamba kwa sababu Serikali Karume ilishindwa kukidhi matarajio ya Wazanzibari wengi, hapakuwa na njia mbadala ila kumwondoa Karume ili kuleta mabadiliko.

Hapa panazuka swali; kama lengo la Hamud la kumuua Karume lilikuwa kulipa kisasi, kwa nini tukio hili lilihusisha watu zaidi ya mmoja? Si hivyo tu; kwa nini watu zaidi ya 1,000 walikamatwa kutokana na mauaji hayo kama haukuwa mpango mpana?
Dhana ya kulipiza kisasi inapungua nguvu kwa kushindwa kusimama kwa miguu miwili. inatuacha njia panda wakati huo ikijaribu kumezwa na dhana mpango wa mapinduzi, kama ilivyodai Serikali.
Inadaiwa kuwa mpango kuipindua, Serikali ya Karume ulibuniwa mwaka 1968 na wanharakati wa mapinduzi ya 1964 wakiwemo raia  na Wanajeshi wachache.
Inasemekana kikao cha mwisho cha mpango huo kilifanyika Aprili 2, 1972 nyumbani kwa Luteni Hamud, ambapo ilikubaliwa kwamba mauaji hayo yafanyike Aprili 7, 1972.
Mpango wa utekelezaji ulikuwa kwamba Hamud na Ahmada wachukue jukumu zito sana la kuiba silaha kutoka Kambi ya Jeshi yaBavuai.

Katika kutekeleza mapinduzi hayo, ambayo mipango na operesheni yake ilifanana kabisa na ya mapinduzi ya 1964, mtu mmoja, Suleiman Sisi, alipewa jukumu la kuongoza mashambulizi kwenye Kambi ya Jeshi la Mtoni na Ahmada alipewa jukumu la Kambi ya Bavuai, Makao Makuu ya Jeshi la Chuo cha Jeshi la Ma­funzo ya Redio ambazo zote ziko eneo la Migombani.

Kambi ya Ubago haikupangi­wa mtekaji kwa kuamini kwamba kama kikosi cha Ahmada kingeweza kuziteka sehemu kili­chopangiwa, Ubago ingesalimu amri sawia.

Kituo cha Polisi Malindi kingetekwa na kikosi ambacho kingeongozwa na Hamud, am­bapo magari yenye redio za mawasiliano yangepatikana kwa watekaji. Ilipangwa kuwa wakati mashambulizi haya yakiendelea, kituo cha Polisi Ziwani kingevamiwa na askari polisi walitarajiwa kuajiriwa na kuongozwa na askari Yusuf Ramadhan.

Mtu mwingine, Amour Dughesh, alipangwa kuteka Ikulu na alipewa jukumu lakumkamata­ Karume na kumpeleka Kituo cha Redio kutangaza kupinduliwa kwa Serikali rake.

Inaelezwa pia kwamba baada ya redio kutekwa, ingewekwa chi­ni ya udhibiti wa Badawi Qual­letein, Miraji Mpatani na Ali Mtendeni. Uwanja wa Ndege ungedhibitiwa na Ali Sultan Issa, ambapo Makao Makuu ya Umoja wa Vi­jana wa AS P (ASPYL) yangetekwa na Baramia.

Makao Makuu ya ASPYL ya­likuwa Kituo Kikuu cha Mkuu wa Usalama wa Ndani ya Serikali ya Karume, Kanali Seif Bakari. Kanali Bakari aliongoza kikun­di cha ukatili kilichojiita kamati ya watu 14, kilichotesa na kuua waliodhaniwa wapinzani na Karume. Abdulrahman Mo­hammed Babu, akiandikia jarida la kila mwezi 'CHANGE' (Vol 4 No. 7,) la 1996, ukurasa 11, anakiri:- "Kutaja pekee jina la Kamati ya Watu 14 kulitosha kumtia mtu woga na kutishika”.

 Kamati hii ili­husika na mauaji ya mamia ya Wazanzibari wasio na hatia, waki­wemo, viongozi, wana’mapinduzi wa kimaendeleo kama Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala, Saleh Saadala, Othman shariff na wengine wale waliuawa kwa jina la Karume."

Abdallah Ameir alipewa jukumu la kuzuia mashambulizi kutoka nje siku hiyo yamapinduzi.
Inadaiwa kuwa katika kikao hicho, Aprili 2, 1972 mtu mmoja, Amar Salim Kuku, alidokeza kuwa Ali Salim Hafidh ambaye nafasi yake haikutajwa katika mpango wa mapinduzi wa Aprili 7, angefi­ka Zanzibar na Abdulrahman Babu na wafuasi wake wa Dar es salaam, usiku wa Aprili 6 kwa mtumbwi kuungana na wanamapinduzi wengine.

Ukiwaondoa Luteni Hamud na Kepteni Ahmada katika mpango huu, na kama ni kweli kwam­ba mpango wote ilikuwa jaribio la mapinduzi (coup d'etat) kama ilivyodai Serikali ya Zanzibar, 'basi staili ya mpango huo haiwezi kut­ofuatishwa na ile ya mapinduzi ya umwagaji damu ya Aprili 12, 1964 ,ambao haukuhusisha jeshi.
Mapinduzi ya 1964 ya kushtukizwa dhidi ya utawala wa Sultan Jamshid na majeshi yake, yali­fanikiwa kwa sababu ya utawala huu kujitenga mbali na wananchi, hivyo haikuweza kupata taarifa za mipango ya mapinduzi hayo mapema.

Na kama ni kweli ilivyosema Serikali ya Zanzibar, kwamba mpango wa mapinduzi ya 1972 uli­buniwa tangu mwaka 1968, ilikuwaje JWTZ na Usalama wa Taifa, achilia mbali kikosi cha Us­alama wa Ndani cha Karume (Gestapo), kilichoongozwa na Kanali Seif Bakari kisibaini mapema hadi siku ya kupoteza uhai wa Kiongozi wa.taifa hilo?  Je, si kweli kwamba historia ya 1964 ilikuwa ikijirudia?

Haya yanaweza kuwa maoni ya wengi, wakiwamo wachunguzi wa mambo ya siasa. Mwanazuoni mahiri barani Afrika, Ali Mazrui anabainisha katika kitabu chake 'Africa's International Relations' (uk. 11); "ukizingatia jinsi Sheikh Abeid Karume alivyoitawala Zanz­ibar kwa ukatili na ubaguzi mkubwa, lolote lilitarajiwa kutokea kwake; hakuna aliyetarajia kwam­ba angedumu kwa miaka minane madarakani. Ndiyo maana hati­maye wengi hawakushangaa alipouawa mwaka 1972."

No comments:

Post a Comment